HIVI NDIVYO NILIVYOANZA KUMFAHAMU MAALIM SEIF – ISMAIL JUSSA

Kwa hakika ni vigumu sana kujaribu kufupisha maisha ya Maalim Seif katika dakika chache, lakini kwa vile umeniuliza jinsi nilivyomfahamu na siasa zake, mimi nilimfahamu Maalim Seif wakati alipokuwa kiongozi.

Wakati huo mimi ni mwanafunzi, na kwa mtu yeyote kama mimi ambaye tangu nina umri mdogo nilikuwa napenda siasa tulikuwa tunafahamu ndani ya chama kimoja wakati huo Chama Cha Mapinduzi wakati ule, Zanzibar kulikuwa na makundi mawili ya kisiasa, na Maalim Seif alikumbukwa sana mwaka 1984 alipokuwa waziri kiongozi wakati wa Ali Hassan Mwinyi aliposhika nafasi ile, watu wengi watakumbuka kuwa licha ya yeye kuwa waziri kiongozi yeye alitajwa zaidi katika siasa za wakati ule na alinasibishwa zaidi na mafanikio ya serikali ya awamu ya tatu kuliko hata aliyekuwa Raisi kwasababu ya uwezo na kipaji chake.

Na nakumbuka katika majarida ya wakati ule “African Events”, kaka yetu Ahmed Rajab aliandika makala akimuelezea Maalim Seif kama kiongozi, alimpa sifa za “Young, dynamic, vibrant and visionary”, (kijana mwenye nguvu ya kutenda, hamihiri mwenye maono) kwahiyo alituvutia wengi wakati huo tupo kwenye maskuli, na ulipokuja mvutano, yaani zilipokuja siasa mpya za awamu ya tatu, walikuwepo wapinzani ndani ya chama kimoja cha CCM. Waliokuwa wakipingana na siasa zile za kimaendeleo wakitaka tubaki kule kule tulipotoka.

Kwahiyo, kukawa na makundi mawili ndani ya CCM maarufu yakaja kujulikana kama ‘Frontliners’ wakiongozwa na Maalim Seif, na ‘Liberators’ ambao ni tabu kusema nani kinara wake, lakini walikuwa wakijumuisha wakati ule kama aliyekuwa waziri kiongozi Ramadhan Haji Faki, Mzee Hassan Nassor Moyo, Abdallah Said Natepe, Ali Mzee Ali aliyekuwa katika baraza la mapinduzi wakati ule na wengine.

Sasa kwa vijana kama sisi na mimi nilipomfahamu tulikuwa tulivutiwa na hawa vijana waliokuwa wakiwakilishwa na Maalim Seif, na baadae kama tunavyojua Maalim Seif hatimae hakuweza kudumu katika siasa za chama cha Mapinduzi kwasababu ya misimamo yake ile, aliondoshwa katika nafasi yake ya uwaziri kiongozi alafukuzwa uanachama wa chama cha Mapinduzi, na baada ya mwaka mmoja tu alikamatwa akafunguliwa kesi za kubuni.

Kwanza aliambiwa amefanya mkusanyiko usio halali na baadae akaambiwa amekutwa na nyaraka za siri za serikali. Sasa kipindi kile alipokuwa gerezani, huku nje ndio kulivuma zaidi umaarufu wake na ndicho kipindi ambacho moja kwa moja mimi nilianza kujiunganisha nae nikiwa ni mwanafunzi wa high school ya Lumumba, kwasababu wengi tulikuwa tukimuita kuwa ni Mandela wa Zanzibar.

Kipindi kile Mandela alikuwa anatambulika kote duniani kuwa alikuwa anapigania haki na uhuru wa watu weusi waliokuwa wanakandamizwa Afrika ya Kusini na akipinga ubaguzi, na ilikuwa ni fakhari kwa Wazanzibari kumnasibisha Maalim Seif na harakati kama za Afrika Kusini, na kwasababu na yeye alikuwa amekamatwa na kuwekwa kizuizini.

Kwahivyo, ilikuwa sote tukienda pale mahakamani na tulikuwa haturuhusiwi kulikaribia gari alilokuwa akiteremshwa lakini kwa mbali atatoa alama ya dole gumba kuashiria alama ya msimamo na tukiingia mahakamani kusikiliza kesi tukiisikia sauti yake akitoa salamu ndani ya ukumbi wa mahakama ikitikisa kuashiria kuwa huyu ni jabari wa siasa za upinzani dhidi ya chama cha Mapinduzi.

Hivyo ndo nilivyoanza kumfahamu Maalim Seif. Lakini baadae, alipotoka gerezani siku ya mwanzo kabisa nilikwenda kumuona nyumbani kwake Mtoni na ndio ikawa mwanzo ya safari ya kisiasa tuloifanya pamoja, na alikuta tayari tumeanzisha harakati za “Kama Huru” ikiongozwa na marehemu Shaabani Khamis Mloo kama mwenyekiti wake, bwana Hamed Seif Hamad kama makamo mwenyekiti, na Mzee Ali Haji Pandu kama katibu wake na tukafanya nae harakati. Hakuchukua nafasi yoyote ndani ya Kama Huru lakini vilipoundwa vyama vingi ikaanzishwa CUF, Maalim Seif aliniita na kuniarifu kuwa nimeteuliwa kuwa katibu wa katibu mkuu wa Chama wakati huo katibu mkuu alikuwa ni Shaabani Khamis Mloo na ikawa ndio mwanzo wa kufanya kazi pamoja, nashukuru nimemfahamu kwa muda mrefu, na yako mengi ya kusema, lakini ninachoweza kusema kwetu sisi alikuwa sio kiongozi tu, alikuwa ni baba mlezi, alikuwa ni mwalimu wetu.

Amelipata jina la “Maalim” kwasababu ya kazi ya kusomesha, lakini likanasibika naye zaidi si kwa kusomesha kwake skuli za Unguja na Pemba lakini ni katika kazi zake za siasa za kusomesha Wazanzibari kisiasa na sisi ambao alitujenga kisiasa na kutuandaa kuwa viongozi wa muda mrefu sana. Hivyo ndivyo ambavyo nimemjua Maalim Seif, nimefanya kazi naye nikiwa katibu wake akiwa Katibu Mkuu wa chama, nimefanya kazi naye katika mazungumzo ya miafaka kwanzia muafaka wa mwanzo uchaguzi wa mwanzo wa mwaka 1995, muafaka wa pili 2000, hadi jaribio la kutafuta muafaka wa tatu ambalo lilikwama Butiama likianzia Bagamoyo 2007 mpaka 2008, na hatimae maridhiano tulofanya yakiongozwa na Rais Karume na yeye Maalim Seif.

Kwahiyo nimefanya kazi naye muda mrefu. Na katika kipindi hicho pia ndie alikuwa akinishika mkono na kuniingiza katika siasa za kitaifa. Ni yeye aliyenambia kazi ya ukatibu basi, sasa ni kuunda tume ya Uraisi ya muafaka kuwa napaswa kwenda katika tume hiyo licha ya mimi kukataa na kusema wapelekwe wengine. Lakini baadae vile vile ulipokuja uchaguzi wa chama na kwa mara ya mwanzo niligombea nafasi za uongozi mwaka 2004 akawa na msukumo mkubwa wa kunifanya niwe mkurugenzi wa mambo ya nje na haki za binaadamu wa chama, na hatimae nikagombea uwakilishi baada ya maridhiano ya mwaka 2009 na 2010, na kazi nyingi ambazo tumezifanya kwa pamoja.

Kwahivyo, naweza kusema kuwa yeye kwangu mimi ni zaidi ya mzee, ni zaidi ya kiongozi, ni zaidi ya Maalim katika shughuli zangu. Hivyo ndivyo ninavyomkumbuka Maalim Seif katika safari ya kisiasa.

Maalim Seif huwezi kumtia ila hata kwa nukta ndogo katika maswala ya ufisadi licha ya kuwa katika madaraka na nafasi za juu kwa muda mrefu sana.

Kuna jambo ambalo Maalim Seif mwenyewe alilitaja katika kitabu chake alichokiandika kinachokusanya kumbukumbu za maisha yake, pamoja na maisha ya Comrade Ali Sultan. Alitaja kadhia ambayo hata mimi binafsi nakumbuka kuwa aliwahi kunieleza, na hata akikaa na jamaa wengine alikuwa anaizungumzia ambayo iliwashangaza wengi.

ZAWADI BINAFSI KUTOKA KWA MFALME WA BRUNEI:

Mwaka 1987 alikuwa waziri kiongozi, alifanya ziara katika nchi za mashariki ya mbali akiitafutia Zanzibar mahusiano makubwa ya kiuchumi, na ndio safari yake ya mwanzo kufika Singapore, hata baadae tukaja tukatafuta idea ya kuja kusema Zanzibar inaweza kuja kuwa Singapore ya Afrika Mashariki.

Lakini safari ile pia ilimpeleka katika nchi (Kisiwa) ya Brunei. Baada ya kukutana na mfalme wa Brunei katika Hijja Makkah, Saudi Arabia. Katika ziara ile, kama tunavyojua Mfalme wa Brunei alitajwa kuwa ni mtu tajiri zaidi kuliko watu wote duniani kwa miaka ile, alimtunuku Maalim zawadi binafsi ya dola milioni tatu ($3,000,000), na alimwambia kuwa hii ni zawadi yako binafsi. Lakini aliporudi fedha zile Maalim Seif aliziingiza katika akaunti ya serikali katika hazina ya Zanzibar.

Alisema kuwa Mfalme wa Brunei hanijui mimi, bali ananitambua mimi kama Waziri Kiongozi wa Zanzibar. Kwahivyo fedha hizi haziwezi kuwa ni zawadi yangu binafsi na siwezi kuzikubali. Na zikaingizwa katika hazina ya Zanzibar. Hakujitajirisha. Alikuwa ni kiongozi kwa zaidi ya miaka arubaini. Hata nyumba za kuishi hana, amebakia kuishi katika nyumba za kukodi. Lakini nyumba yake moja ya Pemba ilibidi ijengwe na kumalizwa na marafiki zake kwasababu ilikuwa inamshinda kujenga.

Hakuwahi hata kujishughulisha kumiliki gari isipokuwa gari ambazo alipewa na chama kutumia kwa ajili ya kazi zake, na mambo mengi kama hayo. Lakini alipoondoka katika nafasi ya uwaziri kiongozi, mwenyewe akisema kulikuwa na jaribio kubwa la kutaka kumchafua, na kuliundwa tume ya kwenda kukagua nyaraka zote katika ofisi za waziri kiongozi kutafuta wapi labda kulikuwa na marupurupu au masurufu aliyoshindwa kurejesha matumizi yake, wakati alikuwa Maalim Seif hata posho za safari alizokuwa akipewa, akirudi hurejesha stakbadhi za matumizi na fedha zilizobakia huzirudisha katika akaunti ya serikali.

KUREJESHA BEGI LENYE FEDHA:

Na la mwisho katika hilo ambalo nataka kulitoa mfano vile vile, wengi hawajalijua kwasababu sijui kama aliwahi kumhadithia mwengine. Katika safari binafsi mara moja alikuwa anakwenda Dubai na alipofika pale alikuwa amechukua briefcase yake, lakini akatokezea mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye alikuwa ana briefcase iliyofanana mno na yake.

Wakati wa kupitisha katika security checkpoint (scan machine) kila mmoja akachukua la mwenzake bila ya kujua. Maalim alinihadithia, alipofiki katika nyumba aliyofikia akalifungua na kukuta limejaa pesa za dola, akajua kwamba sio lake. Jambo hili likamfadhaisha sana. Jambo hili kwa mtu mwengine angelipiga vigeregere kwamba ameokota lulu siku ile.

Lakini yeye alichokifanya katika begi lile ni kutafuta contact za yule mwenye begi. Alipozipata akampigia simu na kumwambia nadhani wewe umechukua begi langu, na yule mtu kwa mshituko akamwambia ni kweli. Alishangaa kuwa mtu alichukua begi lenye fedha na anataka kumrejeshea mwenyewe. Na hakumwambia njoo pahala fulani uje unifuate bali alimwambia kuwa atasogea na vijana wake nusu njia na yeye aende nusu njia ili warudishiane mabegi yao. Huyo ndie Maalim Seif ambaye wengi walishindwa kumfahamu.

KIKAO CHA MSASANI:

Msasani Dar Es Salaam. Nadhani wengi kawaida yetu kuamini katika mambo kama yale labda kwa vile mambo haya hayakusemwa hadharani, kwamba labda kuna kitu kikubwa sana kilichoenda kuzungumzwa.

Kwanza niseme kwamba safari ile ilikuwa ni safari miongoni mwa safari alizokuwa akizifanya mwaka 1993 baada ya kuundwa vyama vingi na CUF kupata usajili wa kudumu. Aliamua yeye wakati ule alipokuwa makamo mwenyekiti akifuatana na wenzake wawili watatu kuwazungukia viongozi mbali mbali wa kitaifa; Jaji mkuu, Spika, na watu wengine mashuhuri akiwemo Mwalimu Nyerere; kwajili ya kwenda kuelezea dhamira ya kuunda chama cha CUF, na nini chama cha CUF kinasimamia. Na mote humo alikuwa akichukua nyaraka za msingi.

Kuna picha maarufu ile ambayo anaonekana akizungumza na Mwalimu. Kwa bahati mbaya ile picha imepigwa wakiwaonesha wawili wao tu kwasababu ndio waliokuwa focus ya mkutano ule. Lakini pia pale alikuwa amefuatana na wenzake. Alikuwa amefuatana na Hamad Rashid Mohammed, Marehemu Mzee Shaaban Khamis Mloo, na Marehemu Khatib Hassan. Na lile linaloonekana katika meza pale, kaprasha nililifunga mimi nikiwa kama katibu wake, ndani yake kulikuwa na katiba ya CUF, muongozo wa sera za CUF, na baadhi za hotuba alizozitoa Maalim Seif zilokuwa zikielezea muelekeo wa kisiasa wa CUF akimchukulia zawadi Mwalimu Nyerere.

Lakini khasa alichokwenda kumwambia alimwambia kwamba tumekuja kwako kukuambia kuwa tumeunda chama, na wewe na wenzako (akimwmabia kwa utani) mmetufukuza CCM, lakini sasa tuna fakhari kuwa vyama vingi vimekaribishwa, na walimshukuru mwalimu kwa mchango wake katika kusukuma ule mjadala wa vyama vingi, na baadae wakawa na mazungumzo mengi walofanya.

Alimtaka mwalimu aingilie kati suala ambalo lilikuwa limeanza la uvunjwaji wa haki za kibinaadamu na kutoheshimu haki za vyama vipya vya kisiasa vilivyokuwa vimeanza. Akamwambia kwa vile wewe ndie ulikuwa kinara wa kusiamamia upande wa CCM kutaka ikubali mfumo wa vyama vingi, sasa ni jukumu lako la kuepuka madhara, ikumbukwe alikwenda kumuona wakati tayari kushatokea mauwaji ya kwanza ya kisiasa Zanzibar kisiwani Pemba Januari 31, 1993 wakati bendera za CUF zilipopandishwa na watu wakapigwa risasi Shumba Mjini.

Mmoja ni Marehemu Omar Haji Ali akafariki dunia na wengine wakajeruhiwa. Akataka mambo kama yale yasijirejee. Vyama viruhusiwe kufanya mikutano ya siasa na bendera zipepee kwa kufungwa kwenye maofisi na mambo mengine.

MAJIBU YA NYERERE KWA MAALIM SEIF:

Jambo moja ambalo linaweza kuwavutia wasikilizaji ni kwamba katika kurejesha majibu Mwalimu alimwmabia kwamba atajitahidi, ingawa alijivua akasema yeye sie tena raisi wa Muungano, lakini angetumia ushawishi wake kulisukuma hilo. Lakini alimwambia kuwa ni kweli nilikufukuza wewe na wenzako, lakini lazima nikiri kuwa haukuwa uamuzi sahihi, na kwamba CCM imepata pigo na imeyumba na imevurugika Zanzibar baada ya kuwafukuza nyinyi lakini mwisho akacheka akamwambia ndio siasa.

Lakini madamu sasa muna chama chenu basi muna haki ya kufanya siasa zetu, na nawaomba mufanya siasa za amani na vile vile muhakikishe kwamba munaulinda muungano. Hiyo ndio iliyokuwa lugha ya mwalimu, na niseme maana labda watu wengi hawakusema hadharani, lakini ndani ya kamati kuu ya chama alikuja akatoa briefing (ufupisho) kamili ya mazungumzo yale, ambayo ndio haya ninayoyakariri mimi ambayo niliyasikia kama walivyoyasikia wengine katika kikao kile cha kamati kuu.

Lakini nataka niseme kwamba moja ya mambo ambayo Maalim atakumbukwa sana na imemjengea heshima sana, na pengine tunajiuliza kwanini mtu anagombea uraisi mara sita, hapewi kuongoza serikali pamoja na kushinda uchaguzi, na bado akirudi kwenye karatasi za kura Wazanzibari wanamiminika kwa wingi zaidi kuliko mara ya mwanzo kumuongezea kura?

Basi kama kuna kitu kinachompa heshima hiyo ni kuwa mkweli katika mambo ambayo aliyaamini, na misimamo yake ya kutoyumba katika anachokiamini. Na hichi tumekishuhudia mara nyingi sisi ambao tumefanya kazi naye, na yameshuhudiwa hadharani kwa vile mambo ya siasa yanakwenda hadharani, lakini pengine wengine walikuwa hawajui nini kilikuwa kinaendelea nyuma ya pazia.

MAZUNGUMZO YA MIAFAKA:

Kuna mambo nataka niyagusie machache. Moja, watu wengi hawajui kuwa masuala ya kuingia katika mazungunzo ya miafaka na maridhiano hayajapata kuwa mepesi ndani ya vyama ambavyo amekuwemo (alipokuwa CUF na hata ACT Wazalendo). Watu wengi wamelitaja hili la karibuni la mwaka jana kwasababu ya namna uchaguzi wenyewe ulivyokwenda, lakini mara zote haijapata kuwa rahisi.

Mimi nakumbuka alipokuja Chief Emeka Anyaoku mwaka 1996 baada ya uchaguzi wa mwanzo wa mwaka 1995, na akaleta package yake ambayo alitaka iwe ndio chanzo cha mazungumzo kupitia shuffling diplomacy kwa maana ya kuwa hakukuwa na mazungumzo ya moja kwa moja, yaani alikuwa anaenda kuzungumza na CCM na baadae anakuja kuzungumza upande wetu sisi tukiwa CUF.

Basi package ile watu wengi waliona kwamba haiakisi kabisa madai yetu kwamba sisi ni washindi wa uchaguzi wa mwaka 1995. Na tuliona kama ile ni jitihada ya kutaka kuisafisha serikali na kumhalalishia ushindi ambao haukuwa wake Dr. Salmin Amour. Lakini Maalim Seif tafauti na sote, yeye aliona fursa, na kwasababu alikuwa anaamini katika kuleta pamoja watu akasema tumepata pa kuanzia, haikuwa kazi nyepesi.

Nakumbuka kikao cha kamati kuu ya chama wakati ule, mimi wakati huo nikiwa katibu tu katika kuweka kumbukumbu katika vikao vya katibu mkuu, lakini nakumbuka jinsi gani alisimama kidete na kujenga hoja ya kwanini tunapaswa kukubali hatua ile ya mwanzo kuelekea katika muafaka, na ilichukua miaka mitatu 1996 mpaka 1999, disappointments zilikuwa nyingi, khiana zilikuwa nyingi sana upande wa CCM, mnakubaliana hili kesho CCM wakirudi wamelikataa, na wamekuja na mengine kabisa na tulikuwa tunekubaliana, hamfiki mwisho, lakini Maalim hakukata tamaa, akaongoza watu, hadi ukapatikana muafaka wa mwanzo.

Na hata pale ambapo haukutekelezwa pamoja na hayo machache yalokuwemo, bado hakuyumba katika kuamini katika ile dhana ya kuwaleta watu pamoja. Lakini hata muafaka wa mwaka 2001 ambao muafaka ule ulikuja baada ya kuuwawa Wazanzibari baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 na maandamano ya 2001, yalitokea baada ya sisi kukubaliana kuwa hakutokuwa na maandamano kwa kusema njia hii inaweza kugharimu maisha ya watu kama ilivyokuwa kawaida ya Maalim Seif siku zote alikuwa akijali maisha ya watu.

Lakini baadae wakati tumesafiri kwenda kufanya kampeni ya kidiplomasia juu ya yale yaliyotokezea, huku nyuma maamuzi yakabadilishwa. Lakini baada ya watu wote viongozi baada ya matokeo yale labda walijificha wengine walikuwa na khofu zao, yeye jabari la kisiasa aliamua kukatisha ziara ile, tulikuwa Uingereza pamoja, akasema yeye anarudi.

Akapita Nairobi kuanza kuonana na waliokuwa wakimbizi, lakini ndie wa mwanzo kupokea hoja ya kuanzisha mazungumzo ya muafaka baada ya kutolewa wito wa mazungunzo wakati watu wake wote wanampinga. Na itakumbukwa mkutano alioufanya Mnazi Mmoja, na Prof. Abdulsharif alikuwa akisema siku zote, katika mikutano yote ya Maalim Seif hajawahi kuhudhuria mkutano mgumu kwake kama ule kutokana na yaliyotokezea lakini bado akakubali mazungumzo ya muafaka ili kuunganisha watu kuipa nchi amani na kusonga mbele.

Lakini kama haitoshi, hata ulipokuja uchaguzi wa 2005 watu wakasema kila siku ni yale yale tu hatutaki tena mazungumzo ya muafaka, Maalim alikuwa mstari wa mbele kutuongoza, tukakaa tukazungumza, mpaka pale CCM walipoamua kuyapiga teke yale makubaliano ya awali.

Na yalipokuja maridhiano vile vile, nakumbuka tulipokwenda hadharani mara ya mwanzo katika viwanja vya Demokrasia pale Kibanda Maiti mjini Unguja, Maalim Seif anazungumza hoja ya kumtambua raisi Karume ili kuweka mwanzo wa msingi wa maridhiano, watu walimzomea kwa mara ya mwanzo, kumtukana na hata kurembea vitu juu ya jukwaa lakini hakurudi nyuma.

Nakumbuka kulikuwa na viongozi wenzetu ambao waliyumba, na ndio hao baadae walishindwa kusimama na sisi na wakatoka kwasababu ya kutokuwa na misimamo wakafanya waliyoyafanya, lakini waliporudi walitaka kumtikisa maalim Seif katika kikao cha tathmini tulichokifanya katika ukumbi wa Mazsons. Na wakamwambia kuwa leo yamekufika haya Unguja, kesho ukienda Pemba ukiyazungumza haya utapata fadhaa kubwa zaidi na unaweza kupigwa mawe.

Maalim Seif akawaambia kuwa ikiwa nyinyi hamuwezi kukabili munachokiamini, nyinyi bakieni. Mimi na wanaonikubali tutakwenda Pemba tukapeleke hoja ya maridhiano. Huyo ndie Maalim.

Na la mwisho hili la juzi mnakumbuka sisi wengine tulikuwa katika vitanda vya hospitali tukiuguza majeraha, lakini alipochukua hoja ile ya kuingia katika serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mara nyengine tena, watu wamemlaumu mno, lakini hatimae nadhani kama ni ushahidi wa faida ya yale wamekuja kuiona, na kila mmoja hata wale waliompinga walikuja kukubali kuwa Maalim aliona mbali.

Kwahiyo siku zote Maalim amekuwa akisimamia anachokiamini, hata kama dunia nzima itampinga akiamini yeye kuwa hichi ni sahihi anasonga mbele.

Na sote akituasa, mara moja mimi aliwahi kunambia, “Ismail unapoambiwa wewe ni kiongozi basi kazi yako ni kuongoza, sio kufuata tu maslahi ya wafuasi kwasababu upepo unawapeleka huku ukaenda nao, kesho upepo ukiwapeleka kule ukaenda nao, wewe utakuwa sio kiongozi, wewe utakuwa ni mfuasi wao. Wao wamekubali wewe uwe kiongozi kwasababu wamekubali your sense of judgement na kukubali kuwa wewe unaweza kuona mbali kwa maslahi yao.” Na hili Maalim Seif alilisimamia.

KUHUSU CORONA:

Na vile vile kuhusu suala la covid wakati nchi nzima ipo katika hatua ya kukataa kwamba hakuna corona, Maalim Seif alikuwa na ujabari wa kutangaza tena hadharani kwamba ameugua maradhi ya corona na ndio kilichoipa ujasiri chama kikatoa taarifa kusema kwamba Maalim ameugua na amelazwa kwasababu hiyo. Kwahiyo huyo ndie Maalim Seif Sharif Hamad, hata katika siku zake za mwisho za uhai wake bado alipoliamini jambo alilisimamia kwa nguvu zake zote. Na mengine mengi tu. Huyo ndie maalim Seif ambaye leo Zanzibar inamlilia. Inamlilia kwasababu sio rahisi kupata kiongozi mwenye msimamo na anayejiamini kama alivyokuwa Maalim Seif.- Ismail Jussa katika mjadala wa maisha ya Maalim Seif.

Tunamuomba Allah amrehemu kiongozi wetu, amlipe mema kwa aliyoyafanya kwa uzalendo na ikhlas ya nchi yake, ameeen.