Nasaha za Dk.Amani Karume kwa CCM

 

Advertisements

Niijuwavyo Zanzibar

Wazazi wangu, Mervyn na Auderey Smithman, walikwenda Tanganyika mwaka 1946 baada ya vita kutokea katika Serikali ya Kikoloni ya Muingereza. Baba yangu alikuwa na cheo cha luteni kanali katika jeshi la kikoloni la Uingereza katika Afrika ya Mashariki (Kings African Rifles). Alitokea Nyasaland (Malawi) na alikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha ya Chinyanja, kwa hivyo aliweza kujifunza lugha ya Kiswahili na kuzungumza kwa ufasaha. Mama yangu alikuwa mwalimu wa masomo ya Jiografia na lugha ya Kifaransa.

Nimezaliwa Mwanza, Ziwa Viktoria ambako ndiyo sehemu ya kwanza baba yangu aliyofanya kazi. Familia yetu iliishi sehemu nyingi za Tanganyika, ambako baba alishikilia nafasi mbalimbali za kisiasa: Bukoba, Biharumulo, Same, Dare es Salaam, Mbeya; na mwishowe tulihamia Zanzibar mwaka 1956.

Katika miezi sita ya awali, tuliishi Pemba ambako baba yangu alikuwa mkuu wa wilaya. Kwenye kitabu cha kumbukumbu za maisha yake, baba yangu anakumbuka vizuri jinsi tulivyoishi maisha mazuri Chake Chake. Kama Mwakilishi wa Serikali ya Kiingereza huko, alihudhuria sherehe ya harusi ya Bwana Hassan Bin Ali Mahadhiy. Baada ya hapo tulihamia Mji Mkongwe, ambapo mwanzoni baba yangu alikuwa kamishna msaidizi mwenye dhamana ya sensa ya watu na makaazi ya mwaka 1958.

Na Anne Chappel

Tuliishi Mazizini kabla ya kuhamia Kikwajuni na miaka yetu ya mwisho Zanzibar tuliishi Shangani pembeni mwa upwa wa bahari, karibu na Mahakama Kuu ya Zanzibar, eneo ambalo lilikuwa zuri kwa watoto. Mimi na kaka yangu tulikuwa na baiskeli na tulikuwa huru kutembea huku na kule. Tuligundua kuwa Wazanzibari ni watu wenye asili ya mchanganyiko mkubwa, wakarimu, wenye furaha pamoja  na uvumilivu.

Nilijifunza kuogelea maeneo yenye mandhari nzuri ya bahari na nilitumia muda mwingi nikifurahia na kujirusharusha katika bahari mbele ya eneo la Mambo Msiige. Tulijifunza kuendesha boti kuanzia bandarini Zanzibar kuelekea Kisiwa cha Changuu na kurudi nchi kavu. Tukikumbuka enzi hizo, tunaona kuwa huo ulikuwa ni muda mzuri kwetu na wa kujivunia. Tatizo kubwa kwetu sisi watoto lilikuwa ni kupelekwa katika skuli za dakhalia.

Kaka yangu, Michael, akawa mchezaji mzuri wa kriketi na alikuwa akicheza katika Klabu ya Wazungu hapo Mnazi Mmoja pembeni ya bahari. Nakumbuka watoto walivyocheza mchezo wa kriketi na baba zao hapo Mnazi Mmoja. Baadaye, Michael alikwenda Afrika ya Kusini kucheza katika timu  za Chuo Kikuu cha Afrika ya Kusini na timu ya Natal “A”. Alitembelea Uingereza akiwa na timu ya wavulana wa Afrika ya Kusini wakiwemo Mike Proctor na Barry Richards; timu za vyuo vikuu vya Afrika ya Kusini na timu ya Colin Wesley. Huko Uingereza alicheza katika uwanja wa Lord’s Cricket dhidi ya timu nyengine nakumfunga Peter May, aliyekuwa Nahodha wa Uingereza.

Mama yangu alikuwa akisomesha somo la Jiographia katika skuli ya Agha Khan kuanzia mwaka 1961 hadi 1962. Mama yangu aliamini juu ya umuhimu wa elimu na naelewa kuwa alichaguwa kufundisha skuli zenye kiwango cha juu.

Kama watoto tulipendelea sana kwenda Majestic kuangalia sinema. Tulikuwa tukinunuwa njugu mbichi kutoka kwa wafanyabiashara nje ya Majestic na pia tukinunua tiketi za sehemu ya juu za sinema.

Nafikiri tiketi ilikuwa ni shilingi mbili. Nafasi za chini zilikuwa ni za bei rahisi sana. Nakumbuka tulivyokuwa tukisiamama ulipopigwa wimbo wa taifa wa Uingereza. Mara nyengine tulikwenda kuangalia filamu za Kihindi na wale waliokuwa wakiangalia sinema sehemu ya chini walitukera pale walipokuwa wakiwapigia makofi wacheza sinema wa Kihindi!

Nilizifahamu sana njia zote za Mji Mongwe. Nilipendelea Mtaa wa Wareno (Mtaa wa Gizenga), mtaa mkubwa ulikuwa na maduka yaliyojaa masonara wa dhahabu, fedha, pembe za ndovu  na baadhi ya vito vya mawe ya thamani kutoka India na Ceylon. Bei zilipanda sana zilipowasili meli za Uingereza.

Baba yangu alijihusisha sana na siasa na ndiye aliyechangia kupatikana kwa Uhuru wa Zanzibar wa mwaka 1963. Mwaka 1959, aliongoza kamati iliyowapa wanawake wa Zanzibar haki ya kupiga kura. Mwaka 1960, aliandika ripoti iliyohusu Maendeleo ya Serikali za Mitaa Zanzibar.

Baba yangu alitakiwa na Sultan wa Zanzibar kusafiri hadi Kisiwa cha Fungu Mbaraka kusini mwa Unguja kwenda kuweka bendera ya Zanzibar kuashiria kuwa kinamilikiwa na Zanzibar. Baba yangu alitunukiwa nishani ya juu na Sultan Sayyid Khalifa bin Harub.

Awali mpango wa Uingereza ulikuwa ni kulekea katika demokrasia pana, lakini kwa vile kipindi hiki kilikuwa cha Vita Baridi kulikuwa na msukumo mkubwa wa harakati za kupigania uhuru kwenye makoloni. Mabishano ya kisiasa yalikuwa ni makali kwa umma. Vyama vikuu vya ZNP/ZPPP pamoja na ASP vilikuwa katika upinzani mkubwa.

Professa J. Glassman anaziita hizi kuwa “Zama za vita vya maneno, vita vya mawe” na hii ilitokana na ukweli kuwa uungwaji mkono wa vyama hivyo ulikuwa ni wa nusu kwa nusu. Hali haikuweza kutabirika.

Baba yangu alikuwa ni msaidizi wa Kamishna wa Tume ya Katiba chini ya Bwana Hilary Blood, wakati alipokuja Zanzibar kupendekeza muundo wa mwisho wa baraza la kutunga sheria. Kwa bahati mbaya, Bwana Blood alitilia mkazo uwepo wa viti 22 vya kuchaguliwa (ambapo kati ya hivyo 8 viti nane vilikuwa ni vya kuteliwa katika hatua hiyo), jambo ambalo lilipekea kuzuka kwa ghasia baada ya uchaguzi wa mwaka 1961.

Mwaka 1962, Waziri wa Uingereza, Bwana Duncan Sunday, alipoitembelea Zanzibar alitangaza kuwa sasa Uingereza ingeliruhusu mfumo mpana wa kidemokrasia. Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1963 yalileta mshangao mkubwa, muungano wa ZNP ulipata ushindi chini ya asilimia hamsini 50% ya kura zote halali – wakati kwa ukaribu waliweza kushinda kwa viti vingi vya majimbo. Baba yangu akateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Waziri Mkuu, Mohamed Shamte.

Sikuwepo Zanzibar wakati wa sherehe za Uhuru wa Disemba 1963 ambapo Mwana Mfalme Phillip alikuwa mgeni rasmi. Wazazi wangu walihusika katika sherehe zote za Uhuru. Mwakilishi wa Uingereza, Bwana George Mooring, aliondoka Zanzbar na ndege pamoja na Gordon Highlandere. Bendera mpya  ya Zanzibar ikapepea.
Nilikuwa nyumbani kwetu usiku wa Mapinduzi wa Januari 12, 1964. Baba yangu alitumia muda mrefu akiwa katika mazungumzo ya simu akijaribu kutafuta msaada wa kijeshi kutoka kwa jirani zetu (Kenya na Tanganyika) na hata Uingereza ambao walikuwa na mkataba wa pamoja wa ulinzi.  Zanzibar haikuwa na jeshi kwa wakati huo. Kwa masikitiko, maombi yote yalikataliwa. Alijaribu pia kutafuta msaada wa jeshi kutoka Pemba, lakini uwanja wa ndege ulikuwa umeshavamiwa.

Nilikuwa na miaka 16 na usiku huo nilitakiwa kukaa juu ya varanda ya nyumba yetu kuangalia makundi yoyote yatakayokaribia katika bustani yetu. Kisa kizima cha matukio haya nimesimulia katika riwaya yangu iiitwayo “Zanzibar Uhuru”.

Wanawake wengine waliokuwemo katika nyumba yetu walisubiri katika eneo la ufukwe wa bahari katika mashua yetu ndogo. Baba yangu alisema kuwa utulivu umerudia ndani ya Mji Mkongwe.

Ilipoonekana wazi kuwa matumaini yote ya kupata msaada kutoka nje yamepotea, baba yangu alikwenda katika Meli ya Salama akitumai kuwa Baraza la Mawaziri lilikuwa huko likiwa kama chombo cha usuluhisi kujaribu kutafuta suluhu na serikali ya waasi. Cha kusikitisha, Baraza la Mawaziri liliukataa ushauri wa baba yangu na likavamiwa.

Hatimaye, Sultan Jamshid na familia yake walikuwa katika meli baada ya kushawishiwa kwa muda mrefu waondoke. Sultan alikuwa anataka kubakia aendeleze mapambano. Baba yangu alisafiri kwenye Meli ya Salama pamoja na Sultan na watu wengine ambao walikataliwa kuingia nchini Kenya. Hatimaye Uingereza ikaandaa mazingira salama yaliyowawezesha kuingia nchini humo.

Matokeo yake ni mauwaji ya kinyama yaliyoongozwa na John Okello yaliharibu kabisa historia ya visiwa hivi.

Kwa kumalizia kisa chetu, familia yetu ilihamia Afrika ya Kusini. Mama yangu alifariki dunia akiwa bado kijana na baba yangu akaowa mke mwengine. Nilikwenda katika Chuo Kikuu cha Durban nilikosomea ualimu, niliolewa na kupata mtoto wa kike na wa kiume. Nilipofika miaka 40, kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe Afrika Kusini na mimi na mume wangu wa pili tulihamia nchini Australia.

Tokea hapo, nimeandika riwaya kuhusu Zanzibar kuelezea historia ya miaka 50  iliyopita. Naamini Wazanzibari waliteseka sana baada ya mwaka 1964. Pia niliandika historia inayohusu maisha ya baba yangu.

Kwa huzuni kubwa, baba yangu alifariki katika makazi yake huko Chester, Uingereza, mwaka 2008 akiwa na umri wa miaka 97. Kwenye droo ya kitandani mwake alikuwa na kasha la karafuu. Baba yangu alikuwa Muafrika kwenye moyo wake, alikuwa mkweli na muaminifu. Alikuwa muhimili wa siasa za Zanzibar, aliyejitahidi kufanya vyema hata katika vipindi vigumu.

Natambuwa namna nilivyobarikiwa kwa kukulia Zanzibar. Sio tu kwa kuwa ni sehemu iliyopendeza na ninayohisi kuwa na muunganiko nayo kwenye siku zangu za utotoni, bali Zanzibar imekuwa pia na msukumo mkubwa katika maisha yangu kwa njia nyengine nyingi.

Makala hii imeandikwa na Anne Chappel (Smithyman), chini ya anuani “MY ZANZIBAR RECOLLECTIONS”, ambaye pia ni  mwandishi wa riwaya ya  Zanzibar Uhuru: Revolution, Two Women and The Challenge of Survival … , anapatikana kwa barua pepe: chappels@bigpond.net.au. Makala hii imetafsiriwa kwa Kiswahili na Mohamed Aliy

Wazanzibari Watumie Nguvu ya Umma kuuondoa Utawala wa Kidiketa Zanzibar

Wasomi wa sheria na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanakubaliana ya kwamba ‘nguvu ya umma’ ni mamlaka ya juu zaidi katika nchi. Kauli hii inaweza kuwashangaza wengi wanaoamini kwamba Katiba ndio mamlaka ya mwisho katika nchi. Bila shaka hilo ni sahihi pia, na yote haya husimama katika mukatadha tofauti. Kwa upande mmoja, dhana ya Katiba kuwa na mamlaka ya juu zaidi katika nchi ni mnasaba katika mazingira ya kidemokrasia ambapo kwa kiasi kikubwa utawala wa sheria unaheshimika. Hivyo, matakwa ya wananchi hupaswa kuzingatia na kufuata mtiririko mzima wa mfumo wa kisheria bila ya kujali matokeo ya mwisho ya madai yao.

Kwa upande mwengine, ni pale ambapo ‘nguvu ya Umma’ inapostahiki kutumika kukiuka mfumo wa kiutawala na sheria kandamizi ili kufikia maslahi mapana zaidi ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko ya haraka ya Serikali. Muktadha huu huweza kutokea ama kwa sbabu Katiba na sheria zilizopo zinakandamiza wananchi, au hutumika kulinda maslahi ya wachache wenye nguvu na madaraka dhidi ya raia. Au sheria hukanyagwa na watawala bila kujali katika kuhakikisha wanabaki madarakani kwa namna yoyote ile. Katika namna hii, ambapo watawala wameigeuza Katiba na sheria zake kuwa kitabu cha hadithi za ‘Alfu Lela Ulela’ kwa kuziheshimu wanapotaka, kuzivuruga wanapotaka, huku wakikandamiza haki za raia bila kujali, kutesa, kuua, na kuligawa taifa, basi ‘nguvu ya Umma’ inakuwa ni mamlaka ya juu zaidi katika nchi. Na ni nguvu ya Umma pekee huwa ndio suluhisho dhidi ya wapiganaji mamluki (jeshi, polisi, usalama wa taifa, na vikosi vya Serikali) ambao hutumika kutia hofu na kukandamiza raia.

Kimsingi, kurudisha mamlaka kwa Umma ndio kanuni kuu ya utawala bora na wa kidemokrasia na ndio chimbuko la Katiba yenyewe na sheria zake zote. Matumizi ya nguvu ya umma hata hivyo huweza kufanikiwa pale ambapo umoja wa kitaifa umeimarika dhidi ya ukabila, ukanda, ubaguzi wa kidini, na matabaka ya kijamii. Wazanzibari wanayo sifa hii ya umoja, hivyo wanao uwezo wa kutumia nguvu ya Umma kujinasua na utawala wa kidikteta. Nitafafanua kwa kina nukta nilizozitaja na nieleze kwa nini Wazanzibari wanaweza kujinasua na utawala wa mabavu wa SMZ.

Watawala wa Zanzibar Wanaitawala Sheria

Dhana ya utawala wa sheria inataka sheria itawale juu ya mamlaka zote na sio watawala kuitawala sheria. Mfano, Serikali kama muanzilishi wa mchakato wa utungwaji wa sheria husika, baada ya sheria hiyo kuanza kutumika, hata serikali yenyewe na viongozi wake wanapaswa kuwa chini ya muongozo wa sheria hiyo. Kwa maana hii sheria si nyenzo ya mtawala kuwatawala watawaliwa, bali sheria hupaswa kuwa juu ya wote wawili yaani mtawala na mtawaliwa. Ndipo waswahili wakasema ‘sheria ni msumeno’.

Kuna kila aina ya ushahidi kwamba Serikali ya Zanzibar na viongozi wake wamekuwa wakiikanyagakanyaga Katiba ya Zanzibar na sheria zake kadri wapendavyo kukidhi utashi wao wa kisiasa. Kwa hapa nitoe mifano michache ya matukio ya hivi karibuni tokea kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba mwaka 2015. Bila shaka tukio la kwanza lilikuwa ni ufutwaji wa matokeo ya uchaguzi kinyume na Katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984. Mamluki mtiifu wa Serikali ya CCM, Jecha Salim Jecha, ambaye watawala wamempendekeza apewe tunzo kwa uharamia wake wa kupindua maamuzi halali ya umma wa Wazanzibari, alijipa mamlaka asiyokuwa nayo yeye binafsi wala tume kwa ujumla wake kufuta matokeo halali na yaliyokuwa yamekamilika ya uchaguzi wa Oktoba 2015. Vyombo vyote vya uangalizi wa uchaguzi, vya ndani na vya nje vikiwemo hata vile kutoka taasisi za Afrika, vilithibitisha kuwa zoezi zima la uchaguzi lilikuwa huru na haki. Cha kushangaza zaidi, tena bila hata aibu, serikali ya CCM ikaamua kunyofoa matokeo ya wabunge na rais wa Muungano kuwa ati yalikuwa yako sawa kutoka katika matokeo hayo hayo yaliyofutwa.

Kiufupi, kila kilichotokea baada ya hapo, kilikuwa ni kinyume na Katiba na sheria za Zanzibar, ikiwemo uchaguzi wa ‘kisanii’ wa marudio wa Machi mwaka 2016, pamoja na Serikali iliyotokana nayo. Pia, msingi mkuu wa utawala wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ulioanzishwa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia marekebisho ya Kumi ya mwaka 2010, ambayo yalipata ridhaa ya wananchi kupitia kura ya maoni, nao ulitupiliwa mbali. Watawala wakaamua kutawala bila kisisi wakidai kutumia Katiba hiyo hiyo, ni kama vile kusoma kitabu kilichogeuzwa maandishi yake juu chini huku unajidai umeelewa. Ni kejeli ilioje kwa utawala wa sheria? Ni dharau ilioje kwa Wazanzibari walio wengi? Hivyo, ni sawa kusema kwamba watawala wa Zanzibar wameitawala sheria, wameikanyaga kwa kisigino. Je haujafika wakati kusimamisha mamlaka ya umma kwa nguvu ya Umma?

Utawala wa mabavu, na vitisho

Wananchi walio wengi katika nchi zilizopitia tawala za kiimla kihistoria ni wenye hamu na ari ya mabadiliko ya mfumo wa utawala. Wazanzibari, hususan vijana na umri wa kati wanakataa kufungamana na siasa za kimirengo ya kihistoria na za kikabila zinazohubiriwa na chama tawala. Hata hivyo, bado raia wengi wa Zanzibar wapo katika hofu kubwa kutokana na ama uzoefu wao wa kihistoria tokea mfumo wa kimabavu wa chama kimoja na utawala wa vitisho wa kimapinduzi, au kutokana na matukio ya hivi karibuni ya uvunjwaji wa haki za binadamu ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Tayari Wazanzibari wamechoshwa na vurugu, ubaguzi, ukandamizaji, na uonevu unaofanywa na Serikali ya SMZ kwa misingi ya itikadi za kisiasa na rangi zao. Pia wamechoshwa na juhudi kadhaa za utatuzi wa migogoro ya kisiasa zilizojulikana kama ‘Muafaka 1’, ‘Muafaka 2’, na ‘Maridhiano’. Juhudi zote hizi zimekuwa zikichukuliwa na serikali ya CCM kwa kebehi na kuvurugwa na kupuuzwa utekelezaji wake. Matokeo yake suluhu hizi zimegeuzwa kama zana za kutuliza hali ya kisiasa nchini ili watawala waendelee kubaki madarakani, na si vyenginevyo. Bila ya woga wala aibu tena katika mazingira rasmi ya kiserikali, viongozi wa SMZ wameendelea kusisitiza kwamba hawatotoa serikali kwa vipande vya karatasi, yaani njia ya chaguzi za kidemokrasia.

Isitoshe, kwa kuelewa kwamba wanayoyafanya ni kinyume na utawala wa sheria na demokrasia, watawala wa Zanzibar wamekuwa wanatumia vyombo vya ulinzi kuwapiga raia wasio na hatia, kuwanyang’anya mali zao, kuwatia hofu, na kuwanyanyasa ili kukandamiza upinzani dhidi ya Serikali. Ripoti za Haki za Binadamu kama vile ripoti ya shirika la haki za binadamu ‘Human Right Watch’ ya mwaka 2002 kuhusiana na Mauaji ya mwaka 2001 imeoredhesha vitendo vya KIGAIDI kabisa na visivyoelezeka kupatwa kutendwa na vikosi vya ulinzi nchini dhidi ya wakaazi wa Zanzibar hususan Pemba. Vitendo ambavyo haviwezi kusahaulika miongoni mwa waathirika. Mengine yakifanywa na vikundi visivyo rasmi maarufu kama Janjawidi kwa baraka ya chama tawala na serikali.

Hivi karibuni, pamoja na uvunjwaji mkubwa wa Katiba na sheria, serikali imeendeleza kutumia vitisho, na kupiga raia kwa kutumia kikundi cha maharamia kijulikanacho kama ‘Mazombi’. Kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu pamoja na kuzorota sana hali ya uchumi kufikia hadi raia wamechoshwa na hali hii. Kimsingi, kiu ya mabadiliko ni kubwa miongoni mwa raia kutokana na kuchoshwa na uonevu. Hata hivyo, Wazanzibari wamekata tamaa na ufanisi wa njia za kidiplomasia za usuluhishi wa migogoro. La kushangaza zaidi, bado wanaendelea kuweka matumaini yao kwa viongozi wa kisiasa hususan wa chama cha upinzani kutumia busara kuweza kurudisha haki yao ya kidemokrasia. Njia ambayo imeonekana kushindwa kufanikiwa kwa muda mrefu sasa na nchi inaendelea kudidimia.

Ni maoni yangu kwamba Wazanzibari wanapaswa waache kuwatwisha jukumu viongozi wa kisiasa na kuwalazimisha watoe matamko ya lipi la kufanya. Wazanzibari wao wenyewe wanao uwezo, umoja, na mshikamano wa kutosha kuweza kuliondoa genge hili la wahuni na wahalifu linaloitawala Zanzibar na kuwanyanyasa raia. Kinachotakiwa ni kujitambua tu. Hata msaada wa kijeshi kutoka Bara ambao umekuwa ukitumika kutishia raia na kuliweka madarakani genge hili, hautaweza kuzima nguvu ya umma ya Wazanzibari wakiamua. Ni wajibu wetu katika jamii miongoni mwa wanaharakati na watetezi wa haki kuanzisha harakati hizi.

Mshikamano wa Kijamii ni msingi wa nguvu ya Umma.

Nilieleza hapo awali kwamba jamii iliyogawanyika kwa misingi ya ukabila, ukanda, na udini ina nafasi ndogo sana kujumuisha nguvu zake kujinasua na utawala wasiouridhia. Kwa mda mrefu sana Serikali ya CCM imekuwa ikijaribu kuwaaminisha watu kwamba Zanzibar kuna tatizo kubwa la ukabila, ukanda, na uvyama. Wakayahubiri haya sio tu katika majukwaa yao ya kisiasa, bali pia katika matendo ya serikali yao na sera zake za kibaguzi. Dhambi ile ile ya wakoloni kutumia rangi ya ngozi kuwabagua watu katika ajira imekuwa ndio falsafa yao kuu ya utawala. Wamekuwa wakitamani kuwagawa Wazanzibari kwa rangi zao, asili zao na maeneo wanayotoka kwa kutumia hivyo kama vigezo vya ajira serikalini. Hata hivyo, kwa mwenye kuifahamu jamii ya Zanzibar vizuri, anaelewa ya kwamba propaganda na sera hizi za kibaguzi hazijafanikiwa kujipenyeza katika maisha ya kijamii Zanzibar.

Kwa mfano, pamoja na kubaguliwa na serikali katika nyanja tofauti, jamii ya Wapemba na watu wenye asili ya Uarabu, hakuna chochote kinachoashiria kwamba jamii imegawika katika misingi hiyo. Wazanzibari ni wamoja na wenye upendo baina yao na muingiliano mkubwa wa kirangi, na kiasili. Ukiwaita machotara, basi Wazanzibari wote katika familia zao ni machotara. Hata hayo makabila maarufu yanayotajwa kuwa ndio ya kizanzibari kama vile ‘wahadimu’, ‘washirazi’, ‘waswahili’ yanapoteza maana kwao, kwa sababu wao hawapendi kujitambulisha na ukabila. Ukimuuliza mzanzibari kabila yake, usishangae akakujibu kuwa kabila yake ni ‘muislam’ au ni ‘mzanzibari’. Kwa sababu dhana ya ukabila haipo katika fikra zao, na makabila wanayonasibishwa nayo kwao wao ni kama misemo tu maarufu hayana maana kwao. Mtu huyo huyo mmoja anaweza kujiita Mhadimu, au Mshirazi, au Mtumbatu, au mswahili, au hata muarabu kwa mujibu wa muktadha aliopo na kutokana na muingiliano mkubwa wa kijamii. Mahusiano yao yameimarika zaidi kutokana na kutokuwepo na migogoro yanayotokana na tofauti ya dini baina yao, kwa vile asilimia zaidi ya 95 ni waislam. Kwa mwenye kubisha akumbuke Wazanzibari walivyoitikia wito wa jumuiya ya Uamsho kuhusu hatma ya nchi yao bila ya vikwazo vya ukabila, rangi zao, wanapotoka, wala mirengo yao ya kisiasa. Zanzibar ilivuma kwa sauti moja.

Pamoja na kufanywa ionekane kwamba Wazanzibari wameweka mbele itikadi za vyama na eti kuna mivutano mikubwa ya kisiasa baina ya wafuasi wa vyama, bado utaifa wao kama Wazanzibari wanauthamini mno. Kimsingi ukichambua itikadi zao za kisiasa utakuta hazishajiishwi katika misingi ya ukabila wala ukanda bali ni matokeo ya matendo ya serikali ya SMZ. Hata hivyo, bado serikali ya CCM inaendelea kupandikiza chuki za kisiasa na zenye madhumuni ya kuigawa jamii bila ya mafanikio. Wazanzibari hawajitambulishi kwa Upemba wao au Uunguja wao, bali wao ni Wazanzibari kwanza kabla ya chengine chochote, hata Utanzania ni kofia ya pili kwao. Na ndio maana serikali ya CCM imeendelea kupoteza imani miongoni mwa Wazanzibari kwa kasi ya kutisha licha ya kujaribu kuficha takwimu hizi kwa wizi wa kura, kuongeza wapiga kura hewa, kuwanyima wenye haki kupiga kura, na kujitangazia matokeo wanayotaka wao. CCM wanafahamu fika ya kwamba Serikali ikishikwa na upinzani na uchafu wote huu kusafishwa, ndipo itajulikana asilimia sahihi ya wafuasi wa chama chao, na bila shaka ni aibu kubwa kwao.

Hitimisho

Nimeeleza kwa ufupi namna gani katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja uliopita Wazanzibari wameshuhudia genge la watawala wa Zanzibar linavyokejeli na kukandamiza utawala wa sheria pamoja na uhuru wa watu. Mbali na uporaji wa wazi wa maamuzi ya kidemokrasia ya Wazanzibari walio wengi juu ya nani awatawale, serikali ya CCM ikaendelea kuwakandamiza raia kwa vitisho, vipigo, udhalilishaji, na kuzidi kudorora kwa hali ya uchumi bila ya kujali.

Ni wazi kwamba ipo sehemu kubwa ya jamii ya Wazanzibari ambao wamekuwa wahanga au waathirika wa vitendo vya serikali ya SMZ kwa kiasi kisichoelezeka. Tumefika kiasi kwamba, hata pakitokea mabadiliko ya utawala itatubidi tuanze na kupoza vidonda vya waathirika hawa kama vile ilivyofanyika Afrika Kusini kupitia mapendekezo ya Kamati ya Upatanishi (Truce Commission) iliongozwa na Askofu Desmond Tutu. Vyenginevyo, tutajenga taifa na jamii ambayo imejawa na visasi kutokana na vitendo vilivyofanywa na wenye madaraka Zanzibar. Jamii ambayo wengine wamepoteza wazee wao na hawakujua makaburi yao yalipo. Jamii ambayo watoto wake wameathirika kwa kupoteza muelekeo wa kimaisha kutokana na wazee wao kujeruhiwa, au kutoweza kuwahudumia kutokana na ulemavu waliopatiwa na serikali. Jamii ambayo watu wake wameshindwa kufikia malengo muhimu kama vile elimu na mahitaji yao kutokana na ubaguzi wa kisiasa, kikabila, na kikanda unaofanywa na serikali ya SMZ. Jamii ambayo sehemu kubwa ya jamii imeathirika kutokana na kutengwa katika utawala na uchumi wa nchi kiasi kuathirika kimaendeleo.

Hivyo, ni dhahiri kwamba Wazanzibari wanazo sababu nyingi za kulazimisha kufanya maamuzi kwa kutumia nguvu ya umma kuleta mabadiliko kutokana na kuchoshwa na utawala dhalimu. Na kutokana na uzoefu wa mda mrefu kuwa njia za utatuzi wa migogoro zimekuwa zikikejeliwa na hazileti mabadiliko yanayotarajiwa, kuna kila sababu ya kukata tamaa juu ya mabadiliko kwa njia ya mazungumzo. Ni wazi kuwa lolote litakalotokea kwa njia ya mazungumzo lazima liwe na maslahi kwa watawala, kinyume chake hawatakubali kuheshimu maamuzi ya Wazanzibari waliyoyafanya mwezi Oktoba 2015 kama yalivyo.

Wazanzibari pia wanazo sifa za kijamii kuweza kuunganisha nguvu ya umma dhidi ya udikteta. Wanao umoja na mshikamano na mapenzi ya taifa lao. Mahusiano yao ya kijamii yamezishinda propaganda za kibaguzi zinazohubiriwa na serikali ya SMZ pamoja na sera zake za kiupendeleo. Wanajitambua kama jamii moja yenye mchanganyiko wa watu wa makabila tofauti na hilo sio tatizo kwao. Ni wajibu wao kutumia mshikamano huu kabla haujavurugwa na hila za watawala wanaozidi kupandikiza chuki na mipasuko kila kukicha.

Nawanasihi wazanzibari tuache kuwangojea viongozi wa kisiasa kututangazia kuandamana kuitoa madarakani serikali haramu ya SMZ. Kilichobakia ni Wazanzibari kuamua kujiondolea dhulma na uonevu wa Serikali ya SMZ wenyewao. Ni wajibu wetu wenye dhima na ushawishi katika jamii kuunganisha nguvu za umma ili kuinusuru Zanzibar isimalizike. Na niwatoe shaka Wazanzibari wanaodhani kuwa idadi yetu ni wachache, kwani historia duniani kote imeonyesha kuwa idadi ndogo tu ya umma uliodhamiria unashinda jeshi lolote lililowahi kuundwa katika ulimwengu huu. Wenye kutaka kurejea historia na wajifunze kutoka mfano wa raia wa Ufilipino walivyoweza kufanya mabadiliko ya utawala mwaka 2001 kwa nguvu ya umma kwa siku nne tu kumtoa rais Joseph Estrada madarakani kama walivyowahi pia kufanya huko nyuma mwaka 1989 kumng’oa dikteta Ferdinand Marcos.

Katika Muktadha wa Zanzibar, sababu tunazo, sifa na uwezo tunao, na hatuna la kupoteza wala kuhofia isipokuwa minyororo ya woga na hofu iliopandikizwa na genge la watawala. Nguvu ya umma ndiyo mamlaka ya juu iliobakia kuinusuru nchi na kusimamisha utawala wa kidemokorasia unaoheshimu maamuzi wa watu, haki za binadamu, sheria na Katiba ya nchi. Njia hii ni njia ya amani, na ni njia ya kidemokrasia inayokubalika na kutumika duniani kuondoa tawala dikteta. Uhalifu wowote utakaofanywa na serikali dhidi ya waandamanaji ikiwemo kumwaga damu za raia katika ulimwengu wa sasa utakabiliwa kwa wahusika kuburuzwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), hususan kwa mazingira ya Zanzibar ambapo mataifa mengi na taasisi zimeshuhudia yaliyotokea oktoba 2015 na wanaendelea kushuhudia ukandamizaji wa haki za binadamu unaoendelea. Macho ya walimwengu yanatuangalia Wazanzibari, tukiridhia tukaachia hili jambo kuwa ni la chama fulani tu, au kuendeleza siasa za vibarazani hatutatoka hapa tulipo. Tufanyeni maamuzi sasa kwa maslahi ya nchi yetu na vizazi vyetu.

By: Mpemba Fyoko